Baadhi ya wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Kata ya Komnyang'anyo wilaya ya Handen ... babarani kuelekea kwenye makazi yao vijiji mbalimbali vinavyoizunguka shule hiyo. |
UJENZI wa Sekondari za Kata katika mikoa mbalimbali umesogeza huduma za
elimu kwa baadhi ya maeneo. Ipo mikoa ambayo awali ilikuwa na shule
chache za sekondari hali ambayo ilifanya wanafunzi wachache kupata fursa
ya kujiunga na sekondari. Kwa sasa hali si hivyo tena, mikoa mingi
imeongeza idadi ya shule hizo licha ya changamoto kibao inazozikabili
shule hizi.
Zipo baadhi ya shule za sekondari zimejengwa mbali kidogo na makazi ya
wahitaji kitendo ambacho huwalazimu wanafunzi kutembea muda mrefu
asubuhi wakielekea shuleni na baadaye jioni wakirejea nyumbani, hali
ambayo ni changamoto kwa wengi wao.
Hata hivyo baadhi ya maeneo shule hizo zimejengwa mbali zaidi na makazi
ya watu kutokana na kile kuhudumia vijiji ama vitatu hadi vinne, na
hazina mabweni jambo ambalo wanafunzi wanashindwa kuvumilia umbali
uliopo kutoka kijiji kimoja hadi kingine hivyo kutafuta mbinu mbadala ya
kusogea jirani na shule wanazokuwa wamepangiwa.
Moja wapo ya Gheto wanazo ishi wanafunzi |
Wanafunzi wanaamua kutafuta vyumba vilivyopo jirani na maeneo ya shule
walizopangiwa na hivyo kupanga (kukodi chumba). Wenyewe vyumba hivi
huviita mageto. Vyumba hivi huwa vidogo na vingine mithili ya vibanda,
ambapo bei huwa ya chini zaidi kwa mwezi. Wanafunzi wengine huamua
kujikusanya wawili ama zaidi na kuishi pamoja kwenye geto ili kupunguza
gharama.
Mkoa wa Tanga katika Wilaya ya Lushoto baadhi ya maeneo aina hii ya
maisha ya wanafunzi ni kitu cha kawaida. Wanafunzi wameamua kupanga
kwenye mageto (vyumba mitaani) na kuishi kwa makundi huku wakikabiliwa
na changamoto lukuki zinazohatarisha safari yao ya elimu ya sekondari.
Mbwambo Conrad ni Mkazi wa Kata ya Bungu wilayani Lushoto, eneo ambalo
lina idadi kubwa ya wanafunzi waliopanga kutoka vijiji vya mbali huku
wakihudhuria masomo yao ya sekondari. Anasema eneo hilo kuna wanafunzi
wengi ambao wametoka vijiji vya mbali na wamepanga jirsni na shule
kwenye kata hiyo kuhudhuria masomo.
Anasema wanafunzi hao wamepangiwa na wazazi wao ili waweze kuhudhuria
masomo yao kuepuka umbali wanaotoka kwenye vijiji vyao. "Wanafunzi hawa
wamepanga katika baadi ya vyumba na wanaishi kwa tabu sana...wengi
wanaingia katika majaribu kutokana na aina ya maisha wanayoishi,"
anasema Mzee Conrad.
Anasema wavulana wengi huishia kuwa wahuni maana uangalizi wa wazazi
hawana, mara nyingi utawakuta wamekaa vikundi kwa vikundi nyakati za
jioni hadi usiku unaweza kufikiri sio wanafunzi. Wanachelewa kulala muda
mwingi wanazunguka kwenye majumba ya sinema (vibanda vinavyo onesha
picha za video) hivyo wanaishi kwa kujitawala utazani si wanafunzi.
Willson N'gwamizi ni Kaimu Mkuu wa Shule ya Sekondari Muungui wilayani
Lushoto, anasema licha ya uwepo wa changamoto mbalimbali katika shule
hiyo suala la wanafunzi kuishi kwenye mageto ni changamoto kubwa kwa
shule kwani linaathiri maendeleo ya shule kitaaluma. Anasema wanafunzi
hulazimika kuishi katika vyumba hivyo vya kupanga kutokana na shule
nyingi za kata zilizojengwa kutokuwa na mabweni huku zikichukua
wanafunzi kutoka vijiji vya mbali.
"...Kifupi suala la wanafunzi kuishi katika mageto linaathiri maendeleo
ya shule kitaaluma...wanafunzi hawa wanapoishi huko hukosa usimamizi wa
wazazi na wengine hata hela ya kumudu maisha hayo huwa ni tatizo maana
wanatoka vijiji vya mbali na uwezo wa familia zao wakati mwingine
hushindwa kuwatimizia mahitaji yote," anasema N'gwamizi.
Anasema kutokana na uhuru huo wa kukaa kwenye mageto wanafunzi wengine
hutoroka na kwenda kufanya vibarua kwenye mashamba ya chai na sehemu
nyingine wasichana nao huwa huru zaidi kitendo ambacho hushindwa
kukabiliana na changamoto za vishawishi mitaani.
"Ukizunguka katika baadhi ya kata unaweza kukuta wanafunzi wa kidato cha
pili wamepanga kwenye chumba kimoja, ndani ya chumba hicho wapo wawili
hadi watatu...wengine wanatoka katika familia duni hawapewi mahitaji ya
kutosha, wengine hujikuta wanashawishika na kuingia mitaani na kujikuta
wanakatizwa masomo kwa kutiwa ujauzito," anasema.
"Kwa kweli mageto ni tatizo, wapo baadhi ya walimu hujitahidi
kuwafuatilia huko wanakoishi ili kuhakikisha wanajenga nidhamu ya
kiuanafunzi, hata hivyo zoezi hili bado ni changamoto maana na walimu
wamejikuta wakikaa mbali na shule kutokana na ukosefu wa nyumba za
walimu jambo ambalo ni tatizo pia...," anasema mwalimu huyo.
Suala la ukosefu wa mabweni kwa shule za kata na kuwalazimu wanafunzi
kupanga mitaani (mageto) halipo kwa wilaya ya Lushoto pekee. Wilaya ya
Handeni nayo inakabiliwa na changamoto hiyo ya wanafunzi kupanga
uswahilini wenyewe karibu na shule walizopangiwa.
Ester Frank ni mmoja wa wanafunzi wa sekondari za kata wilayani Handeni
anasema changamoto kwa wanafunzi kukaa kwenye mageto ni kubwa hasa wa
kike. Anasema wengi wanakosa uangalizi na usimamizi hivyo kujikuta
wanajiingiza kwenye vishawishi hivyo kuishia kupata mimba na kukatizwa
masomo yao. "...Usema kweli mageto yanatuathiri wanafunzi hapa wilayani
Lushoto," anasema mwanafunzi huyo.
Afidha Said ni mkazi wa Kijiji cha Kidereko, Wilaya ya Handeni, mkoani
Tanga. Said anasema katika mahojiano na mwandishi wa makala haya
kijijini Kidereko wilayani Handeni, aliyekuwa akifuatilia vitendo vya
ukatili wa kijinsia ambavyo hufanyiwa baadhi ya wanafunzi na wanawake
eneo hilo kwa ushirikiano na Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania
(Tamwa). Anasema matukio ya mimba kwa wanafunzi eneo hilo si kwamba
hulazimishwa kimahusiano, bali huingia wenyewe katika mahusiano kingono
kutokana na mazingira halisi.
Anasema ukiachilia mbali uduni wa kipato kwa familia nyingi eneo hilo,
ambao wengi ndio wazazi/walezi wa wanafunzi, shule nyingi za kata Wilaya
ya Handeni zipo mbali na makazi ya wanafunzi. Zimejengwa hivyo ili
kuweza kuhudumia vijiji vingi, ambavyo pia kuna umbali mkubwa kutoka
kijiji kimoja hadi kingine.
Wapo wanafunzi ambao hulazimika kutembea kilometa 12 hadi 20 kwenda na
kurudi shuleni kila siku jambo ambalo linawaumiza wengi, hivyo
kulazimika ama kutafuta urahisi wa kupata usafiri hasa kwa wanafunzi
wanaotoka vijiji vya mbali au kulazimika kupanga katika mageto jirani na
shule walizopangiwa. kwa usafiri maarufu ambao hutumika na jamii maeneo
mengi ya vijiji hivi ni pikipiki (bodaboda), ambao wazazi hawawezi
kuumudu kwa wanafunzi wao kutokana na gharama za juu.
Mmoja wa walimu katika moja ya shule za kata wilaya ya Handeni (jina
tunalihifadhi kwa kuwa si msemaji) anasema shule yao inawanafunzi
wanatoka katika vijiji kama Kidereko ambacho ni takribani kilomita 6
kwenda na Kijiji cha Bangu ambacho ni karibu kilomita 10 kwenda tu.
Anasema umbali kama huu ukiuunganisha mwanafunzi analazimika kwenda na
kurudi kila siku unakuta ni tatizo.
Anasema na wengi wanatoka katika familia duni unakuta hawapewi chochote
wanapotoka nyumbani kama matumizi ya siku (kula), sasa katika hali kama
hii inakuwa tabu. Wapo ambao wanaamua kukata tamaa ya kuendelea na shule
hivyo kujiingiza katika mambo ambayo yanawaharibu kitabia kabisa.
Rais Jakaya Kikwete akihutubia wananchi Januari 7, 2013 mjini Igunga
aliwahi kusema kuwa serikali inajitahidi kukabiliana na changamoto za
elimu. "Kwa upande wa elimu tumeendelea kupata mafanikio katika
kupunguza tatizo la upungufu wa walimu wa shule za msingi na sekondari.
Mwaka huu (2013) tuliajiri walimu 28,666. Kwa ajili hiyo upungufu wa
walimu ni 57,755 kati yao 20,625 wa shule za msingi na 37,130 wa shule
za Sekondari.
Rais Kikwete anasema kwa mwaka 2014 Serikali itaajiri walimu wapya
36,100 kati yao 18,100 wa shule za msingi na 18,000 wa sekondari.
Kufanya hivyo kutafanya pengo lililopo liwe dogo zaidi. Kwa upande wa
shule za sekondari, tatizo la walimu wa masomo ya sanaa tunakaribia
kulimaliza. Changamoto yetu kubwa itakuwa kwa walimu wa masomo ya
sayansi.
Rais Kikwete anasema upungufu ni walimu 26,998 na uwezo wa vyuo vya
ualimu nchini ni kutoa walimu wa sayansi 2,300 kwa mwaka. Anaongeza kuwa
mapema mwaka 2014 Serikali itakutana na wadau wa elimu nchini
kujadiliana juu ya mkakati wa haraka wa kulikabili tatizo hilo.
Hata hivyo licha ya juhudi hizi kwa upande wa changamoto ya walimu hasa
kwa shule za kata kuna haja ya Serikali kuangali namna ya kulipa
kipaumbele suala la kupambana na changamoto za umbali wa shule za kata
na makazi ya wananchi na kuhakikisha ujenzi wa mabweni ili kupunguza
adha wanazopata wanafunzi wa kike na kiume kutokana na changamoto hiyo
inamalizima kama si kupungua kwa kiasi fulani. Tukiamua tunaweza
kukabiliana na changamoto hizi.
Like Page Yetu Hapa Kuungana Nasi Facebook
0 comments:
Post a Comment