Mwalimu Galus Focus Nguruwe akiwa amefungwa mnyororo
Ndugu
wa mtu anayedaiwa kuwa ni mlemavu wa akili, Galus Focus Nguruwe (35)
ambaye ni mwalimu wa sekondari moja mjini Morogoro, wamelituhumu Kanisa
la House of Prayer Shield of Faith Christian Fellowship lililopo Boko Magengeni jijini Dar kuwa wamemfunga mnyororo ndugu yao huyo kwa miezi nane mfululizo.
Kwa
mujibu wa dada wa Galus, Piencia Focus, ndugu yao huyo alichukuliwa na
mke wa mtoto wa dada yao waliyemtaja kwa jina la Doreen kutoka Songea
mkoani Ruvuma Januari, mwaka huu bila kuwataarifu ndugu, jambo
lililowafanya wamfuatilie na kugundua alipelekwa kwenye kanisa hilo kwa
madai ya kufanyiwa maombi.
Dada
huyo alisema kuwa aliamua kumtafuta ndugu yake hasa baada ya kupata
taarifa kuwa aliko amekuwa akishinda huku amefungwa mnyororo mguuni,
hali inayomfanya ajisaidie na kula papohapo.
“Japokuwa
alikuwa na matatizo ya akili tangu zamani, lakini alikuwa akitumia dawa
zake na alipata nafuu na kufanya kazi yake ya ualimu kwani alikuwa
akifundisha shule moja ya sekondari Morogoro,”
alisema Piencia Focus.
Kaka wa Galus,Peter Focus akizungumza na waandishi wa habari.
Naye kaka wa Galus, aliyejitambulisha kwa jina la Peter alisema baada
ya kupata taarifa kwamba mdogo wake yupo kwenye kanisa hilo aliamua
kufika kwa ajili ya kumchukuwa kistaarabu lakini cha kushangaza
alijikuta akiangukia kwenye mikono ya waumini hao wakidai yeye ni gaidi
na wakamkwapulia fedha zake.
Peter alisema alipoachiwa alikimbilia Kituo cha Polisi Wazo Hill ambapo alifungua jalada lenye Namba za Kumbukumbu WH/RB/6364/14 WIZI TOKA MAUNGONI.
Peter alisema alilazimika kuungana na dada yake kwa kushirikisha na vyombo vya usalama ambapo walifika kanisani hapo kwa mara nyingine ili kumkomboa ndugu yao na kuwatia mikononi waumini waliomwibia fedha zake.
Waandishi
wetu waliokuwa karibu na eneo hilo walizinyaka taarifa hizo na kufika
kanisani hapo ambapo waliwashuhudia ndugu hao wakiwa na polisi
wakimchukuwa mmoja wa watuhumiwa waliodaiwa kumshambulia Peter na
kuondoka naye.
Hata
hivyo, jambo la kushangaza ni kitendo cha polisi hao kumwacha Galus
akiwa bado amefungwa kwenye nguzo na mnyororo kanisani hapo wakidai
watamfuata baada ya kumpeleka mtuhumiwa wa unyang’anyi kituoni, jambo
ambalo halikuwa la kweli kwani hawakufika kwa siku hiyo.
Waandishi
wetu walishuhudia timbwili la aina yake kanisani hapo kati ya waumini
wa kanisa hilo na ndugu wa Galus waliorejea kwa lengo la kumchukuwa
ndugu yao baada ya awali kumpeleka kituoni mtuhumiwa wa kumshambulia
Peter.
Waandishi
wetu walipoomba kuzungumza na uongozi wa kanisa hilo ilishindikana na
kujikuta wakishambuliwa kwa maneno huku wakitakiwa kuondoka mara moja
katika eneo la kanisa hilo.
ANKO SAM BLOG.
Like Page Yetu Hapa Kuungana Nasi Facebook
0 comments:
Post a Comment