Sunday, 1 June 2014

Ufafanuzi wa mofu katika maneno

Nida, (1949). Kama alivyonukuliwa na Mgullu, mofu ni umbo la neno ambalo huwakilisha mofimu na ambalo hudhihirika kifonolojia na kiothografia. Mofimu ambazo ni elementi dhahania huwakilishwa na mofu ambazo hudhihirika ama kifonolojia zikiwa ni sauti za kutamkwa au kiothografia zikiwa ni alama za kuandikwa.
Hivyo basi, mofu ni kipashio cha kimofolojia kiwakilishacho mofimu.
Kwa kuzingatia ufafanuzi huu, ni wazi kabisa zinaelezea mambo ya msingi kuhusu sifa muhimu zinazopambanua dhana ya mofu. Sifa hizo ni pamoja na:
Mofu ni sehemu halisi ya neno. Ni wazi kuwa, mofu ni maumbo halisi ya maneno ambayo hutamkwa wakati watu wanapozungumza au kuandikwa wakati watu wanapoyaandika (Mgullu, 1999).
Mofu hudhihirika kifonolojia na kiothografia. Kutokana na kuwa mofu ni umbo halisi la neno, basi mofu mbalimbali hudhihirika kifonoljia zinapotamkwa na pia kimaandishi zinapoandikwa (Mgullu, 1999).
Mofu huwakilisha maana. Msisitizo hapa ni kwamba, mofu huwakilisha maana. Kwa hiyo, katika neno lolote katika lugha yeyote panakuwepo maana na maana hizo huwa zimesetiriwa katika mofu zilizopo katika neno. Hata hivyo, kuna maneno mengine ambayo hayana mofu. Kwa mfano, maneno kama vile Baba, Mama na Kaka. Maneno haya ni huru hivyo hayawezi kugawanyika zaidi (Mgullu, 1999).
Mofu ni kipashio kidogo kabisa cha neno chenye maana. Hapa kinachotiliwa mkazo ni ule ukweli ya kuwa mofu ni sehemu ndogo kabisa ambayo hubeba maana na kwamba sehemu hiyo haiwezi kugawanywa katika sehemu ndogo zaidi zilizo na maana (Mgullu, 1999).
Bauer, (1983). Kama alivyonukuliwa na Mgullu, alomofu ni mofu mojawapo katika seti ya mofu zinazowakilisha mofimu fulani ambayo ina mazingira yake ya kifonetiki, kileksika au kisintaksia.
Ufafanuzi huu unaelezea sifa muhimu zinazoifafanua alomofu. Sifa hizo ni pamoja na alomofu ni umbo, ambapo ni umbo halisi ambalo ni sehemu ya neno fulani na ambalo hutamkwa na kuandikwa. Alomofu ni mofu mojawapo miongoni mwa mofu za mofimu moja. Tofauti inayojitokeza hapa ni kuwa mofu huwa ni mofu wakati ambapo umbo moja tu hutumika kuiwakilisha mofimu fulani (Karanja, 2004).
Kwa hiyo, alomofu ni umbo mojawapo kati ya maumbo kadhaa tofauti yanayowakilisha mofimu moja.
Ufuatao ni ufafanuzi wa mofu au alomofu zilizo katika maneno yafuatayo na aina zake:
Mamake.
{mamake}- ni umbo la nje.
{mama} {yake}- ni umbo la ndani.
Kwa hiyo, neno mamake lina mofu mbili, yaani {mama} na {yake} ambapo, {mama} ni mofu huru na {yake} ni mofu changamano, lakini mofu {ke} ni mzizi tegemezi, kwa sababu {ya} inaweza kubadilika. Kwa mfano, zake.
Kuta.
Neno kuta lina mofu mbili, yaani {Ø} kapa na {kuta}.
Mofu ya kwanza ni kapa {Ø}.
Mofu {kuta} ni mzizi funge.
Chezea.
Katika neno hili kuna mofu tatu, yaani {chez}, {e} na {a}.
{chez-} ni mzizi tegemezi wa kitenzi.
{-e-} ni alomofu tegemezi na tata ambayo inaleta dhana ya kutendea.
{-a} ni alomofu tegemezi ambayo ni kiambishi tamati yakinishi.
Wanahewa.
Neno hili lina mofu mbili, yaani {w} na {anahewa} ambapo,
{w} ni mofu tegemezi, wakati
{anahewa} ni mofu changamano ambayo imeundwa na mizizi miwili, yaani {ana} na
{hewa}.
Mwanagenzi.
{mwanagenzi}- ni umbo la nje, wakati.
{muanagenzi}- ni umbo la ndani.
Neno hili lina mofu mbili yaani, {mu}- ni mofu tegemezi na mofu {anagenzi}- ni mofu changamano ambayo imeundwa na mizizi miwili ambayo ni {ana} na {genzi}.
Hivyo basi, ili kupambanua dhana ya mofu au alomofu, inakupasa utambue sifa zinazopambanua dhana hizi mbili, lakini pia uweze kutambua umbo la nje na la ndani la neno husika ili kuweza kubainisha vema mofu au alomofu zake zinazounda neno husika.


MAREJEO
Habwe, J na Karanja, P (2004). Misingi ya Sarufi ya Kiswahili. Nairobi: Phoenix Publishers
Mgullu, R. S (1999). Mtalaa wa Isimu: Fonetiki, Fonolojia na Mofolojia ya Kiswahili. Dar es
Salaam: Longhorns Publishers.

Like Page Yetu Hapa Kuungana Nasi Facebook

0 comments:

Post a Comment